VITALI MAEMBE KUWANIA UBUNGE BAGAMOYO



 Hatimaye Mwanamuziki Nguli anayefanya muziki wa Asili Maembe Vitali "Mswahili" Leo amefunguka rasmi kwa umma kuwa ameamua kujitosa kuomba kujiunga na chama chochote cha siasa ili kiweze kumpa ridhaa ya kugombea nafasi ya Ubunge katika Wilaya ya Bagamoyo.


 Kupitia mitandao ya kijamii Maembe amesema kuwa, yeye si mwanachama wa chama chochote cha siasa, na kwa kuwa sheria za nchi yetu aziruhusu mtu yeyote kugombea bila kupitia chama chochote (Mgombea binafsi), ameamua kuweka wazi Itikadi zake ili kama kipo chama kitakachozikubali basi kiweze kumkaribisha na kumpa ridhaa hiyo.

 Maembe ameeleza kuwa yeye ni mjamaa na anaamini kuwa binadamu wote ni sawa na yupo kinyume na ubaguzi wowote wa rangi, dini, Kabila na vilevile yupo kinyume na ubaguzi wa Aina yeyote unaodunisha Utu wa mtu, na kusisitiza kuwa "hawezi kubadilika kwenye hilo".

 Pia mkali huyo wa vibao "Sumu ya Teja", "vuma ","kudu" na nyinginezo, ameeleza pia yeye ni Mwanamuziki wa umma hivyo anatarajia chama hicho kitamruhusu kuendelea kuufanya Muziki wake kwa Uhuru kwa watu kwenye muda wake.

 "Ninaishi na kuamini kuwa Rushwa ni Adui wa Haki na Maendeleo. Hivyo kukubaliwa kwangu na chama chochote kutaniaminisha kuwa majukumu nitakayopewa hayatanilazimisha kwenda kinyume na Itikadi hiyo, na ntajitolea kuwa Mtumishi mwaminifu kwa Viongozi wa chama hicho na kuheshimu Katiba ya Chama na Katiba ya Nchi"alisema Maembe.

 Nguli huyo aliongezea kuwa, Kama ikitokea hajakubaliwa na chama chochote isichukuliwe vibaya Kwani katika kuomba kuna kupewa na kunyimwa,na Sio kila kunyimwa kuna maana mbaya.Lakini Hata hivyo hatua hiyo itamfanya kuendelea na mapambano na utaratbu uleule mpaka nchi itakaporuhusu "mgombea Binafsi" na muda utakaporuhusu.



Comments

Popular posts from this blog

MWANAMUZIKI MAARUFU AACHA MUZIKI KWA MSONGO WA MAWAZO